Posted: Wednesday July 18, 2012 5:38 AM BT

TAFITI mbalimbali zimekuwa zinafanywa na wataalamu wengi katika nyanja tofauti za kiuchumi ili kuona ni kwa namna gani mwananchi anaweza kujikomboa kutoka kwenye lindi la umaskini.

Mathalani ukipitia tafiti kadhaa za mashirika na asasi mbalimbali zinazojishughulisha na upunguzaji wa umaskini nchini na kuwajengea uwezo wa kipato wananchi, utabaini kuwa yako mambo kadhaa ambayo yanakosekana kwa walengwa.

Lipo suala la mitaji ya fedha, teknolojia ya kufanyia uzalishaji wao, masoko ya kuuza bidhaa zinazozalishwa pamoja na elimu ndogo ya ujasiriamali ya kutambua ni biashara ya aina gani inaweza kufanyika, wakati gani na mahali gani.

Hivi karibuni Shirika la Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), lilifanya utafiti katika maeneo kadhaa ya uzalishaji jijini Dar es Salaam na kubaini kuwa ujenzi wa makundi ya viwanda unahitajika kusaidia ukuaji wa makampuni na viwanda vidogo vidogo ili kupunguza umaskini.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Repoa wanasema mipango maalumu inahitajika ili kuongeza ukuaji wa viwanda vya useremala katika sehemu mbalimbali zenye viwanda hivyo nchini.

Utafiti huo uliofanywa kwenye makampuni ya utengenezaji wa samani yasiyo rasmi jijini Dar es Salaam, umeainisha changamoto wanazokumbana nazo wamiliki na wafanyakazi wa makampuni hayo kuwa ni pamoja na kuwa na ujuzi mdogo wa biashara, miundombinu mibovu ndani ya viwanda hivyo, teknolojia iliyopitwa na wakati, na upatikanaji mbaya wa malighafi.

Utafiti huo ulioitwa “Ukuaji wa viwanda vya kati na vidogo, na makampuni ya kutengeneza samani na matokeo yake katika kupunguza umaskini nchini Tanzania”, unatoa wito wa kusaidia ukuaji wa viwanda vya samani kwa kupatiwa mipango maalumu ili kuboresha ngazi za uongozi za makampuni hayo na viwango vya bidhaa zao.

“Kufikia ngazi ya juu ya sekta ndogo ya viwanda kuna ulazima wa kuwapo kwa ukuaji wa makampuni ya samani,” alisema Edwin Mhede, mwandishi wa utafiti huo.

Alibainisha kuwa ukuaji huo unategemea uboreshwaji wa uongozi wa makampuni hayo na uboreshwaji wa viwango vya bidhaa zao ili kukidhi matakwa ya soko la hapa nchini, kikanda na kimataifa.

Uchunguzi ulifanywa kwenye ukuaji wa makampuni madogo na yale ya kati ya kutengeneza samani yanayofanya kazi katika sehemu tatu za Dar ea Salaam za Keko, Buguruni-Malapa na Mbezi Beach kwa Komba.

Pia utafiti huo ulitazama jukumu la sehemu hizo katika ukuzaji wa makampuni hayo ya samani na uhusiano uliopo kati ya ukuaji huo na upunguaji wa umaskini kwa wafanyakazi na wamiliki wa makampuni hayo.

Matokeo ya utafiti huo ulionyesha kuwa kwa wastani makampuni ya samani hukua katika masuala ya ulipaji wa wafanyakazi wao na jinsi yanavyowanufaisha wamiliki wa kampuni hizo.

Pia makampuni hayo yalionekana kufaidika na kuwepo katika sehemu zilipo na walikuwa wanafahamu faida hizo.

Hata hivyo kulikuwa na ukosefu wa ukuaji wa ongezeko la ajira katika muda wote wa utafiti, ingawa asilimia 62 ya wamiliki wa makampuni waliosailiwa walisema kuwa maboresho yametokea katika hali yao ya maisha kwa ujumla.

“Kati ya sehemu zote zilizofanyiwa utafiti, wamiliki wa kampuni za Mbezi Beach kwa Komba wameonesha kuona mabadiliko ya hali yao ya maisha, ikifuatiwa na Buguruni-Malapa na Keko,” alisema Mhede.

Kwa upande mwingine, wafanyakazi wa Kampuni za Buguruni-Malapa ndio wameonyesha kuona mabadiliko ya uboreshwaji wa maisha yao wakifuatiwa na waajiriwa wa Keko na Mbezi Beach kwa Komba.

Utafiti ulipendekeza kuwa uanzishwaji wa biashara na ujengaji wa sehemu za viwanda, hifadhi na kanda kama njia ya sehemu hizi kusaidia ukuaji wa kampuni hizo za ili kupunguza umaskini Tanzania.

“Hiyo itazidi kuwapa moyo kampuni za samani ambazo tayari zimefanikiwa katika kuboresha viwango vya bidhaa, utafutaji wa masoko, na uongozi kuhamia kwenye sehemu maalumu za viwanda,” alisema Mhede.

Ni wajibu wa serikali sasa kuvutia viwanda vinavyotengeneza bidhaa zinazofanana na kuhusiana kuhamia katika sehemu hizo maalumu za kufanyia biashara.

This article was published in the Tanzania Daima newspaper and is also available at the following link: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=38254
recommend to friends
  • Google+
  • PrintFriendly